
MSHAMBULIAJI hatari wa Al Ahly ya Misri inayotarajiwa kuvaana na Yanga katika mchezo wa raundi ya 16 ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Malick Evouna, rekodi yake ya kucheka na nyavu imezidiwa na ‘muuaji’ wa Jangwani, kijana mpole asiye na mbwembwe uwanjani na nje ya uwanja, Amissi Tambwe.
Evouna amekuwa akitajwa kama mchezaji wa kuogopewa kutokana na uwezo wake wa kucheka na nyavu, lakini wastani wake wa kufunga mabao kulingana na mechi alizocheza ukiwa ni mdogo kuliko ilivyo kwa Tambwe.
Wakati Evouna akiwa na wastani wa mabao 0.4, Tambwe ni 0.8, ikiwa ni mechi za timu zao za Ligi Kuu za nchi zao msimu huu.
Kwa upande wake, Evouna amefunga mabao saba ndani ya mechi 15 alizocheza msimu huu kwa mujibu wa mtandao wa fifa.com, wakati Tambwe akiwa amecheka na nyavu mara 17 ndani ya mechi 21 za kikosi cha Yanga.
Ukiachana na msimu huu, hata misimu iliyopita rekodi zinaonyesha Tambwe ni zaidi ya Evouna katika kufunga mabao kwani Mgabon huyo akiwa na kikosi cha Wydad Casablanca, wastani wake wa mabao ulikuwa ni 0.4, wakati alipokuwa katika kikosi cha Mounana ni 0.7.
Tambwe akiwa Simba wastani wake wa mabao kulingana na mechi ulikuwa ni 0.7, wakati alipotua Yanga dirisha dogo la msimu wa 2014/15, alifunga mabao 14 ndani ya mechi 13, hivyo kuwa na wastani wa bao 1.07.
Kutokana na takwimu hizo, inaonyesha kuwa Tambwe ni hatari zaidi katika suala zima la kutumbukiza mipira nyavuni dhidi ya mpinzani wake huyo raia wa Gabon.
Ukiachana na Evouna, mchezaji mwingine wa Al Ahly ambaye ni hatari katika kufunga mabao, ni El Said Abdallah ambaye naye amefunga mabao saba ndani ya mechi 21, wakati kwa upande wa Yanga anayemfuatia Tambwe ni Mzimbabwe Donald Ngoma aliyetikisa nyavu mara 13 baada ya kushuka dimbani mara 21.
Kwa ujumla, washambuliaji hao wawili wa kutegemewa wa Al Ahly wamezidiwa shabaha za kufunga mabao na wenzao wa Yanga, kwani wakati wao wakiwa na wastani wa mabao 0.3 wenzao wa Jangwani, jijini Dar es Salaam ni 0.7.
Pamoja na hayo yote, bado Evouna ameonekana kuwa mchezaji hatari mno ambaye anahitaji kuchungwa mno na kukabwa kwa umakini na mabeki wa Yanga, kwa mujibu wa vipande vya video zake zinavyopatikana You-Tube, akiwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, mbio, chenga, nguvu na mwenye shabaha ya kulenga goli, japo wakati fulani ameonekana kuwa na papara mno anapokuwa katika eneo la hatari.
Kama ilivyo kwa Tambwe, Evouna ni hodari wa kufunga kwa vichwa na miguu yote, akiwa pia ni mmoja wa wapigaji penalti tegemeo wa Al Ahly.
Muuaji mwingine wa Al Ahly, Abdallah, yeye amekuwa akicheza kama Tambwe kwamba si mpambanaji kama ilivyo kwa Evouna na Tambwe, kazi yake ikiwa ni kusubiri mipira imdondokee au kuwekewa pasi kwenye njia akamalize kazi.
Kutokana na hali kama hiyo, ni wazi kuwa katika suala zima la kufunga mabao, Tambwe ndiye mwenye nafasi zaidi ya kuwatungua Al Ahly iwapo ataamka vizuri siku hiyo na kutuliza akili zake, huku mabeki wa Yanga wakitarajiwa kuwa makini mno kumdhibiti Evouna, lakini pia kutomsahahu Abdallah ambaye anaonekana ni kama ‘Mzee wa Kuvizia’.
Mchezo baina ya timu hizo mbili utapigwa Aprili 9, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya miamba hiyo kurudiana wiki mbili zijazo jijini Cairo, Misri ambapo mshindi wa jumla atatinga hatua ya makundi.
Credit:Bingwa