Uongozi, wanachama na mashabiki wa Jang’ombe Boys ambao wamepanda ligi kuu visiwani Zanzibar kwa msimu wa 2015-2016 leo Jumamosi wanatarajia kumpokea kocha wao kutoka Uturuki ambaye anatarajiwa kutua visiwani humo mchana.
Rais wa Jang’ombe Boys, Ally Othman amesema, maandalizi yote kwa ajili ya mapokezi ya kocha huyo yameshakamilika wanachosubiri ni muda tu ufike ili wamlaki kocha wao.
“Leo (jana) tumekwenda kwa OCD wilaya ya Mjini kupata baraka za kutumia njia na kupata ulinzi kwa ajili ya mapokezi ya kocha wetu ambaye atafika hapa siku ya kesho (leo) majira ya saa 8:30 mchana kwa boti ya Super Sea Bus”, amesema Othman.
“Kocha akishuka tutaranda nae, tutakuja nae mpaka kijijini kwetu Jang’ombe, baada ya kumpokea na akishazungumza na wanakijiji baadae tutampa ruhusa ya kwenda nyumbani kwake ambako atakuwa akiishi nje ya mji (VIP Area au Chukwani)”.
“Lengo letu ni kutengeneza timu yenye ushindani na si ya kushiriki”.