Gor Mahia imekuwa timu ya kwanza kutinga kwenye hatua ya robo fainali kwenye michuano ya Kagame Cup baada ya kuibuka na ushindi kwenye michezo yake miwili kwenye Kundi A, kundi pekee lenye timu tano kwenye michuano ya Kagame. Gor Mahia waliibuka na ushindi wa goli 2-1 kwenye mchezo wao wa ufunguzi kwa kuifunga Yanga na leo wameitwanga KMKM goli 3-1 na kuongoza Kundi A kwa kuwa na pointi sita huku wakiwa wamefunga magoli matano wakati wao wamefungwa magoli mawili.



KMKM ilijitahidi kucheza vizuri kipindi chote cha kwanza lakini makosa madogomadogo yaliwakosesha ushindi. Walijitahidi kutengeneza nafasi za kufunga lakini walishindwa kuzitumia nafasi hizo kupata mabao. Licha ya kupiga mpira mwingi leo, Juma Mbwana Faki alikosa goli akiwa amebaki yeye na kipa, Mateo Saimon na yeye pia alipoteza nafasi kadhaa za kufunga.
Mbali na kukubali kichapo hicho cha magoli matu, KMKM ilionesha mpira mzuri hasa kipindi cha kwanza na kuwapa matumaini wadau wengi wa soka la Tanzania huenda wakaweza kuutafuna mfupa uliomshinda Yanga lakini kipindi cha pili mambo yalibadilika na kujikuta wakiruhusu magoli mawili.
Olunga mpaka sasa ameshafunga magoli matatu baada ya kucheza mechi mbili. Mchezo wa kwanza alifunga goli moja wakati timu yake ikicheza dhidi ya Yanga na leo ametupia kambani goli mbili na kuipeleka timu yake kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Mchezo uliotangulia (saa 8:00 mchana), Khartoum ya Sudan iliibuka na ushindi wa kishindo kwa kuicharaza Telecom ya Djibouti kwa goli 5-0.