Kocha mkuu wa Mbeya City FC 'Wanakoma kumwanya', Meja Mstaafu Abdul Mingange anaendelea na program zake za mazoezi kwenye uwanja wa Sokoine jijini hapa tayari kwa mchezo ujao wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Mgambo JKT uliopangwa kuchezwa kwenye uwanja huo jumapili ijayo.
Kocha Mingange amesema kuwa baada ya kumalizika kwa mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar aliandaa mpango maalum ili kuwaweka fit wachezaji wake na anaamini mechi itakuwa ngumu kutokana na matokeo ya sare waliyopata wapinzani wake katika mchezo wao uliopita.
“Nina program maalumu kuhakikisha tunapata matokeo dhidi ya Mgambo, najua kuwa walipata sare dhidi ya Yanga mchezo wao uliopita, hii ina maana kuwa walitumia nguvu nyingi dhidi ya timu hiyo kubwa, ndiyo sababu tunafanya aina hii ya mazoezi ya mbinu ili tuwe na uhakika wa matokeo” alisema.
Katika hatua nyingine katibu mkuu wa City, Emmanuel Kimbe ameweka wazi kuwa usajili wa nyota wanne uliofanywa mapema baada ya dirisha dogo kufungwa ndiyo pekee uliofunga kipindi hiki cha usajili mdogo huku wachezaji wawili, Medson Mwakatundu na Rajabu seif wakiwa wamepelekwa kwa mkopo kwenye tmu ya Geita Gold ya Geita.
“Abdallah Juma,Deo Julius,Ditram Nchimbi na Tumba Sued Lui ndiyo wachezaji wapya kwenye kikosi chetu katika kipindi hiki cha dirisha dogo,huku Medson Mwakatundu na Rajab Seif wakiwa wamepelekwa kwa mkopo Geita Gold,hiyo ndiyo kauli pekee naweza kusema katika kipindi hiki” alisema katibu Kimbe.