KOCHA wa Mabingwa wa ligi ya Ujerumani, Bundesliga, Bayern Munich, Pep Guardiola, ameripotiwa kuwa mwishoni mwa Wiki hii atatangaza rasmi kutoendelea na Klabu hiyo baada ya Msimu huu kumalizika.
Mkataba wa sasa wa Guardiola na Bayern unamalizika Mwezi Juni na licha ya wakali hao wa Allianz Arena kutaka kumpa Mkataba mpya Kocha huyo kutoka Hispania, aliekuwa na Barcelona kwa mafanikio makubwa mno, amesita kusaini huku kukiwa na ripoti atatua Jijini Manchester ambako haijulikani ni Etihad au Old Trafford.
Hata hivyo, Wadadisi wanahisi ipo nafasi kubwa sana ya kutua Manchester City ambako uongozi wa Meneja Manuel Pellegrini unakisiwa kutoridhirisha Wamiliki wa Klabu.
Akiwa na Bayern, Guardiola aliiongoza Klabu hiyo kutwaa Ubingwa wa Bundesliga mara 2 lakini mara 2 alitupwa nje na Klabu yake ya zamani Barcelona, Mwaka 2014 na 2015, kwenye UEFA CHAMPIONZ LIGI.
Msimamo huu wa Guardiola wa kutotaka kusaini Mkataba mpya mapema unasemekana umeikera Bayern ambayo imedaiwa tayari imeshakubaliani na Carlo Ancelotti kushika hatamu Msimu ujao.
Ancelotti aliondolewa Real Madrid mwishoni mwa Msimu uliopita na sasa hana kazi ingawa mwenyewe amedokeza kutaka kurejea kibaruani Msimu ujao.