
Jonas Mkude
LICHA ya kushinda bao 1-0 na kuvunja rekodi ya kutowahi kuifunga Mbeya City tena ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani, bado Simba haijaridhika na matokeo hayo, badala yake imeamua kuwaweka kitimoto wachezaji wake watano.
Simba imewaweka kikaangoni wachezaji wake hao kwa tuhuma za kucheza chini ya kiwango katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine Jumamosi iliyopita.
Waliojikuta matatani ni mabeki Hassan Kessy na Hassan Isihaka pamoja na viungo watatu Jonas Mkude, Abdi Banda na Mwinyi Kazimoto.
Juzi Jumanne katika mazoezi ya timu hiyo ambayo yalikuwa ni maandalizi ya mechi yao dhidi ya Prisons iliyochezwa jana (Jumatano) baadhi ya wanachama ambao wapo jijini hapa wakitokea Dar es Salaam walimvaa Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Collin Frisch kumtaka azungumze na wachezaji hao ili watoe msimamo wao ndani ya timu hiyo.
Mwanaspoti ilishuhudia kikao hicho kifupi kilichofanyika uwanjani hapo, wakati timu ikiendelea kufanya mazoezi huku ikielezwa kwamba wachezaji hao wanapaswa kuonywa ama kutafutiwa mbadala ili wapate changaoto ndani ya kikosi chao.
"Tulipata ushindi lakini timu ilicheza chini ya kiwango hasa kwa baadhi ya wachezaji, tumemwambia Collin akae na wachezaji hao awaeleze ili tujue tatizo lao ni nini na kwa nini wanacheza chini ya viwango.
"Kuna wachezaji kama Isihaka, Kessy, Mkude, Banda na Kazimoto wapo ndani ya timu na hawajitumi," kiliongeza chanzo hicho na kusisitiza kuwa:
"Banda na Mkude sawa wametoka kwenye majeraha lakini kweli kwa mfano Mkude ambaye alikuwa anategemewa leo hii ndiye anayeongoza kwa kucheza chini ya kiwango, inaumiza sana, nafikiri viongozi watakaa na wachezaji hao ili wajue matatizo yao ni nini halafu tutajua cha kufanya, Collin ametuahidi kulifanyia kazi."
Hata hivyo, kitaalamu mchezaji anayetoka kwenye majeraha hawezi kucheza kwa kasi kama walivyokuwa hapo awali, hivyo Banda na Mkude kasi yao ni lazima itakuwa ndogo kama hakuna sababu nyingine.