Baada ya kuifunga timu ya Mbeya City, Wekundu wa Msimbazi wameshindwa kutamba leo kwenye uwanja wa Sokoine mbele ya Tanzania Prisons kufuatia kupokea kichapo cha goli 1-0 mchezo uliomalizika jioni ya leo.
Goli pekee na la ushindi kwa upande wa Tanzania Prisons ‘wajelajela’ limekwamishwa wavuni na Mohamed Mkopi katika dakika ya 62.
Ushindi huo unakuwa ni wanne kwa Prisons ambayo imeshinda michezo mitatu nyumbani huku ushindi wake wa ugenini ukiwa ni dhidi ya Kagera Sugar walioibuka na ushindi mnono wa goli 3-0 kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.
Mwishoni mwa juma lililopita Simba ilifanikiwa kushinda kwa mara ya kwanza mbele ya Mbeya City kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya tangu timu hiyo ilipopanda daraja kucheza ligi kuu Tanzania bara.
Kufungwa kwa Simba leo hii, kunawafanya wawe wamepoteza mchezo wa pili msimu huu, mchezo wao wa kwanza kupoteza ulikuwa ni ule dhidi ya watani wao wa jadi Yanga uliopigwa Septemba 26 mwaka huu.